Post by Admin on May 20, 2015 17:06:19 GMT
Alikuwepo mama mmoja aliyekuwa chongo, mwanae alimchukia kwa sababu ya kuwa chongo. Mwanae alijisikia aibu kufuatana na mama yake mwenye jicho moja na hakupenda watu wajue kuwa yule ni mama yake.
Hata alipokuwa shuleni hakupenda mama yake amtembelee, na ikitokea mama yake akamtembelea basi watoto wenzie watamcheka siku nzima na kumtania. Hii ilimfanya mtoto huyu kujisikia vibaya sana na wakati mwingine kujuta kuwa na mama wa aina hiyo.
Lakini mama alimpenda mwanae na hakuonesha kukasirika hata pale mwanae alipomnyanyapaa waziwazi.
Badae mtoto akakuwa, akamaliza masomo yake na kupata kazi nzuri. Akafurahi kuwa sasa amepata kazi atakuwa mbali na mama yake 'chongo' anayemtia aibu.
Akachagua kufanya kazi mji wa mbali na alipo mama yake. Akafanikiwa kazini kwa kupandishwa cheo na akawa mtu mashuhuri mwenye mali na mwenye heshima kubwa ktk jamii yake.
Siku moja asubuhi akasikia wanae wakilia walipokua nje wakicheza, alipowauliza wakasema kuna mtu anawatisha. Akatoka nje kujua nani anayewatisha wanae. Kufika akamkuta mwanamke mmoja mzee mwenye jicho moja (chongo). Kumbe wale watoto walitishwa na chongo la yule bibi.
Alipomtazama vizur yule mwanamke akamgundua ni mama yake mzazi. Alikua amechoka na amezeeka sana. Amedhoofu mwili na anaonekana mgonjwa.
Mtoto kwa hasira akamuuliza "mama umekuja kufanya nini hapa, kama una shida ungenipigia simu sio kuja? kwanza nani kakuonesha napoishi? Na nani kamruhusu mlinzi kukufungulia mlango?" "...ona sasa umewatisha wanangu kwa chongo lako."
Mama yake akasema; "Samahani mwanangu, sikujua." Kisha mtoto akamchukua mama yake akamtoa nje na kumpeleka kituo cha basi ili arudi kijijini.
Baada ya siku chache kupita, yule jamaa akapata taarifa kuwa mama yake ni mgonjwa sana na anahitaji kumuona. Akaondoka kwa siri kwenda kijijini ili akasikie mama anataka kumwambia nini.
Alipofika akakuta watu wengi wamekusanyika nyumbani kwao. Alipouliza akaambiwa mama yake alifariki baada ya kuugua sana bila msaada wowote.
Alipoingia ndani akakuta barua aliyoandika mama yake. Barua ilisomeka hivi...
"Kwa mwanangu mpendwa wa pekee.Naandika barua hii nikiwa kwenye maumivu makali sana na sijui kama nitapona... Nimeugua nikakosa matibabu kwa kutokuwa na fedha. Sikuwa na mtu mwingine wa kumueleza shida yangu zaidi yako wewenangu wa pwaee... Lakini nilipojitahidi kuja kwako angalau unisaidie matibabu ulinifukuza na kudai nawatisha wanao kwa chongo langu."
"Baba yako alifariki ukiwa mdogo sana, nami sikubahatika kupata mtoto mwingine. Nilikulea kwa nguvu zangu zote nikitegemea badae utanisaidia lakini umenitelekeza na kunitupa kwa sababu tu mimi mama yako ni chongo, hivyo unaona aibu kuwa karibu nami."
"Nisamehe kwa kuwatisha wanao kwa chongo langu, nisamehe kwa kuja kwako bila taarifa, nisamehe kwa kukufanya uchekwe na wenzio kwa kuwa mimi mama yako ni chongo."
"Lakini naomba nikupe siri ambayo hukua unaijua. Mwanangu wewe ndiye uliyezaliwa chongo, ulikua na jicho moja tu. Nikaumia kuona mwanangu una jicho moja, utawezaje kuishi na kukabiliana na changamoto za maisha. Nikaomba madaktari wanitoe jicho langu moja wakupe wewe. Niliona ni heri mimi niwe chongo kwa kuwa nimeshaona mengi sana duniani kuliko wewe."
"Na ulipowekewa jicho langu nilifurahi kukuona una macho mawili nikajua utaweza kuzikabili vema changamoto za dunia hii. Na hakika jicho langu limekusaidia kwani wewe ni mtu mashuhuri na tajiri sana kwa sasa."
"Lakini kwa jinsi ninavyoumwa najua nitakufa. Ila nafurahi kuwa nakufa nikiwa nimetimiza haja ya moyo wangu, kwa kutumia jicho langu umeweza kuwa msomi mzuri na tajiri unayeheshimika na jamii yote. Wasalimie wajukuu zangu na waambie wawe na amani hawataniona tena nikienda kuwatisha na chongo langu...please take care of my eye."
Akupendaye,
Mamayo chongo."
Alipomaliza kuisoma barua hii akalia sana. Akatamani mama yake afufuke amuombe msamaha na amlipe kwa wema wake aliomtendea. Lakini haikuwezekana. It was TOO LATE.!
MORAL OF THE STORY.!
Nyuma ya mafanikio ya kila mwanaume yupo mwanamke. Anaweza kuwa mama yako, mke wako au dada yako. Je unatambua nafasi yake katika mafanikio yako au unampuuza tu?
Wapo wanawake ambao walijitoa sadaka ili uweze kuwa hapo ulipo. Jiulize mama yako amefanya mangapi kukufikisha hapo.
Hadithi hii inatueleza juu ya mama aliyetoa jicho lake kwa mwanawe. Lakini jicho ni kielelezo tu cha yale wanayofanya mama zetu.
Kuna wengine jicho lao ni vibarua alivyokua anafanya mama ili wewe usome. Pengine jicho lake ni namna alivyokua akijinyima kwa kuvaa nguo moja mwaka mzima ili upate ada ya shule na mahitaji mengine. Je umewahi kumshukuru mama yako kwa kutoa jicho lake kwa ajili yako?
Mpende sana mama yako. Wapende wanawake wote. Waheshimu, walinde, wajali. Wanapitia magumu mengi sana ili kutufanya sisi wanaume tuwe kama tulivyo.