Post by Admin on May 31, 2015 21:25:53 GMT
Mama Kaguba alilia kwa uchungu,
japo haikufaa
kitu. Wakarejea kwenye teksi yao
na kusubiri
kadari ya Mungu tu iwakute
maana hawakuwa na
namna nyingine.
Walikaa pale bila ya kupata
msaada mpaka jioni
ikawakuta wakiwa palepale huku
hofu, mchoko na
njaa vikizidi kuwashambulia.
Ndipo ghafla
wakatokea vijana wawili waliovaa
nguo chafu na
chakavu wakiwa wanakusanya
kuni.
“Habari zenu jamani?” Kungurume
aliwasalimu
vijana wale baada ya kuteremka
kwenye gari na
kuwasogelea. Akiwa na dada yake
kwa pembeni.
“Nzuri tu…” walijibu vijana wale.
“Jamani samahani tunahitaji
msaada wenu…sisi
tumeharibikiwa na gari na tupo na
mgonjwa aliye
mahututi sasa tunaomba tafadhali
mtudaidie
jamani?”
“Mnakwenda wapi na huyo
mgonjwa wenu?”
“Tunampeleka kwa mganga mmoja
hivi anaitwa
Babu Gao.” Jibu hilo la
Kungurume likawafanya
vijana wale waangaliane kwa
udadisi.
“Dereva wenu yuko wapi?” Aliuliza
mmoja kati ya
vijana wale wawili.
“Dereva aliteremka ili kuangalia
hiyo hitilafu
iliyotokea, cha ajabu hatukumuona
tena akawa
ametoweka.” Jibu hili alilitoa
mama Kaguba, japo
inaonekana alimkera kaka yake
kwa kusema jambo
hilo ambalo lingeweza kuwatisha
na kuwaacha na
maswali mengi zaidi badala ya
kuwapatia msaada.
“Mnh!” aliguna kijana mmoja.
“Nd’o yuleee?” kijana mwingine
akamsaili
mwenziye ambaye alitikisa kichwa
kuashiria
kukubalialichoulizwa.
“Iko hivi jamani…” Alianza
kuongea kijana
aliyekuwa na upanga mkononi
mwake. “…Sisi ni
vijana wa huyo Babu Gao
mnayemfuata, huku
tulikuja kusanya kuni na kuwinda
kitoweo lakini
muda mfupi tu uliopita
tumekutana na kijana
mmoja amevaa kofia nyekundu
akatuambia kuwa
amepotezana na wenziye na
kwamba yeye ni
dereva teksi…itakuwa nd’o huyo
eeh?” Safari hii
sasa ikawa zamu ya Kungurume
na Mama Kaguba
kutazamana kwa mshangao.
Hii ndiyo faida ya kuwa mkweli
maana kama
Mama Kaguba angedaganya basi
pengine vijana
wale wasingejua kisanga hicho
kuwa kinahusiana
na huyo kijana waliyemuona.
“Nd’o huyohuyo alikuwa amevaa
kapelo
nyekundu.” Jibu la hilo kutoka
kwa Mama Kaguba
likamfanya kijana mmoja atoke
mbio akielekea
porini kujaribu kumtafuta huyo
dereva waliyekutana
naye.
“Huyu mgonjwa wenu atakuwa
amerogwa vibaya
sana…” Alianza kuongea kijana
aliyebaki na akina
Mama Kaguba wakati mwenziye
amekimbia mle
porini. “…maana si ninyi tu, bali
wengi wakiwa
wanakuja kwa Babu hupotea
ghafla au
kuharibikiwa safari mpaka
wanaamua kurejea huko
mjini. Ila ondoeni shaka hata kama
gari itaharibika
basi tutambeba mgonjwa wenu
kwenye miti mpaka
tutamfikisha kwa Babu, na hata
hapa tulipo bila
shaka Babu atakuwa amekwisha
tuona kupitia
‘Tivii’ yake ya asili.”
“Yaani hata hatuamini kama
tumepona aisee,
ahsanteni sana. Kwahiyo ninyi ni
wajukuu kabisa
wa Babu Gao?”
“Naam, mi’ ni mjukuu wake kabisa,
mtoto wa wa
mwanaye. Ila huyo aliyekimbilia
huko porini ye’ ni
Kanumba(msaidizi’ mganga) wake.
Wakiwa wanaendelea kupashana
habari, ndipo yule
aliyekimbilia porini akarejea akiwa
na yule dereva
teksi. Maongezi yakafa kwanza!
Hapakuwa na haja
ya kupiga soga tena, wakaingia
kwenye teksi kisha
yule Kanumba akatoa dawa fulani
na kuimwagia
teksi…na kumuamuru dereva
awashe gari.
Kama mchezo wa kuigiza vile, gari
ikakubali na
safari ikaanza. Ndani ya teksi
walibanana wote.
Akina Kungurume na mgonjwa
wao, pamoja na
wale vijana wa Babu Gao.
Kumbe wala hawakuwa mbali sana
na nyumbani
kwa Babu Gao kwani muda mfupi
wa safari
waliwasili na kumkuta Babu gao
akiwa amejipinda
na shughuli ya kutengeneza mipini
ya majembe.
Wakateremka kutoka garini na
kumsogelea Babu
Gao, cha ajabu Babu aliendelea na
shughuli zake
kama hajawaona wageni licha ya
muungurumo wa
gari yao kuvuma tangu wanaingia
eneo lile, hali
hiyo iliwashangaza si tu akina
mama Kaguba, bali
hata wale vijana wake walihisi
kitu.
“Babu shikamoo!” Mama Kaguba
na Kungurume
walimsalimu Babu Gao.
“Marahaba,” aliitikia salaam ile
Babu Gao huku
akishindwa hata kukitaabisha
kichwa chake japo tu
kuwatazama.
“Habari za hapa?” Mama Kaguba
alisaili kwa
fadhaa.
“Nzuri.” Babu aliendelea kujibu ki-
mkato.
“Babu tumekuja na mgonjwa yumo
ndani ya gari…
ni mjomba Mtandi amepoteza
fahamu kabisa.”
“Sasa?”
“Tumekuja kwako Babu tunaomba
msaada wako!”
“Amepotezea wapi fahamu?”
alisaili Babu Gao.
“Tangu nyumbani…ilikuwa hivi
alikuwa akitu…”
Kabla mama Kaguba hajamalizia
kauli yake
akakatizwa na Babu Gao.
“Sasa fahamu amezipotezea huko
kwenu halafu
mnakuja kuzitafutia kwangu! Mi’
siwezi kuzipata
naomba muondoke haraka
tafadhali nina kazi
nyingi za kufanya.”
Heeh…!
“Babu siye ni wajukuu zako, au
umetusahau?”
“Sina wajukuu kama ninyi…na
kama ni wateja
wangu ni kwamba sihitaji kufanya
kazi nanyi
kabisa jamani mwende au mpaka
niwafanyie kitu
kibaya?”
Laiti kama mzee Mtandi angekuwa
na fahamu
angetambua ukweli wa kile
alichokisikia kwa binti
Sambayu akimueleza Kaguba
kuwa wamemtisha
na hata kutaka kumuhonga Babu
Gao ili aache
kufuatilia kesi hiyo hivyo
yawezekana mganga
huyu amesalimu amri.
Babu Gao alikuwa amebadilika
kabisa na kuwa
kama hajui lolote kuhusu wageni
wale. Kama
haitoshi Babu akanyua uso wake
ili awakaripie
vijana wake tabia za kuokota watu
huko na
kuwaleta pale kwake. Alipoinua
sura yake tu kabla
hajawakaripia vijana wake
akakutanisha macho
yake na nyuso zilichoka na kukata
tamaa kabisa
kutoka kwa Kungurume na Mama
Kaguba.
Waswahili wanasema wao kuwa
Ukitaka kumuua
Nyani, usimwangalie usoni…
utamuonea huruma.
Hivyo ndivyo ilivyokua kwa Babu
Gao alijikuta
akishusha pumzi za huruma.
Badala ya kukaripia
kama alivyokusudia, badala yake
akawaambia
vijana wake waondoke ili abakai
na wageni wake.
Vijana wakaondoka!
“Sikilizeni jamani…jambo lenu ni
kubwa sana na
limenielemea kiasi cha kutishia
maisha yangu…”
Alianza kuongea Babu Gao baada
ya kuweka
pembeni zile zana zake alizokuwa
akizitengeneza.
Akawaelezea kwa kirefu ugumu wa
suala lao lile,
akawapasha habari jinsi
alivyofuatwa na kutishiwa
maisha yake na wafuasi wa
Kaguba na mambo
mengine mengi tu.
Mjadala ulikuwa mpana sana.
Akina mama Kaguba
walimlilia babu na kusaga meno ili
awasaidie
mpaka hatimaye Babu Gao
akalegea. Akawaambia
wamteremshe mgonjwa kutoka
ndani ya gari kisha
wamuingize ndani. Vijana
wakaitwa kusaidia zoezi
lile.
Baada ya kukamilisha zoezi hilo,
Kungurume
akamlipa dereva teksi na
kumwacha aende zake
kwani kwa mujibu wa mganga,
wao walipaswa
kulala palepale. Kuwafahamisha
nyumbani kwao
haikuwa tabu kwani tangu
walipofika kwa Babu
hapo mtandao ulikuwa ukifanya
kazi.
***Haya!
ITAENDELEA...